Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na ujumbe wake na wenyeji wakiongea na wanahabari na kisha kupiga picha ya pamoja baada ya Mazungumzo yao Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili. |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili
nchini Kenya Jumanne, 11 Septemba , 2012, kuanza Ziara Rasmi ya Kiserikali (State Visit)
ya siku tatu ikiwa ni ziara yake ya kwanza rasmi nchini humo ingawa ameshawahi kufanya
ziara kadhaa za kikazi nchini Kenya.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Rais Kikwete
ambaye amefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, amepokewa na mwenyeji wake,
Rais Mwai E. Kibaki na kwa mbwembwe zote za kiprotokali zinazoambatana na ziara
rasmi za kiserikali.
Baadaye
mchana, Rais amekwenda Ikulu ya Kenya ambako ametia saini kitabu cha wageni,
akafanya mazungumzo ya faragha na Rais Mwai Kibaki kabla ya kufanyika kwa
Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili majirani na wanachama wa
Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Baada
ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete na ujumbe wake amekwenda kwenye Chuo Kikuu cha
Kenyatta ambako wamepokewa na Waziri wa Elimu ya Juu, Mheshimiwa Margaret Kamar,
Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Onesmus Mutungi na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa
Olive Mugendi.
Kwenye
chuo hicho ambacho Desemba 8, mwaka 2008, kilimtunuku Rais Kikwete Shahada ya
Uzamivu ya Heshima, amefungua rasmi Jengo la Shule ya Ukarimu na Utalii ya Chuo
hicho.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Shule hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utalii ni sekta
muhimu sana katika chumi za nchi za Afrika Mashariki na ambayo mchango wake
unagusa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wa nchi za ukanda huo.
Rais
pia amesema kuwa nchi hizo za Afrika Mashariki sasa zimekuwa ni eneo lenye
mvuto mkubwa katika nyanja ya utalii ambao unaweza kuwaingizia wananchi na
mataifa ya Afrika Mashariki mapato zaidi kama changamoto zinazoikabili sekta ya
utalii kwa sasa zitashughulikiwa ipasavyo na kwa pamoja na nchi hizo.
Miongoni
mwa changamoto ambazo Rais Kikwete amezitaja ni ukosefu wa miundombinu ya
kutosha kufanikisha kwa namna bora zaidi sekta ya utalii, ukosefu wa juhudi za
pamoja kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo muhimu la utalii, na umuhimu wa
kuboresha kiwango cha usalama wa watalii.
Aidha,
Rais Kikwete amezielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na umuhimu wa
kuwepo na viza ya pamoja ya utalii kwa nchi zote za Afrika Mashariki, kuwepo
kwa safari za ndege za kutosha kutoka kwenye mataifa makubwa yanayozalisha
watalii kwa wingi kuja Afrika Mashariki na umuhimu wa kupungua kwa nauli za
ndege za kuja Afrika Mashariki.
Jioni, Rais Kikwete ametembelea Taasisi ya Utatifi wa Kilimo ya Kenya (KARI)
ambako anatarajiwa kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Kenya, Mheshimiwa Dr.
Sally J. Kosgei na usiku alikuwa mgeni rasmi kwenye Dhifa ya Kitaifa ambayo itaandaliwa
na mwenyeji wake, Rais Mwai Kibaki.
Leo Jumatano 11 Septemba, 2012 Rais Kikwete ataweka shada la maua kwenye Kaburi la Mwanzilishi wa Taifa la
Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, kwenye Viwanja vya Bunge la Kenya na kutembelea
Kiwanda cha Maziwa cha Brookside Diary kwenye Barabara ya Thika.
Kwa
mujibu wa ratiba ya ziara yake, Rais Kikwete atatembelea Chuo cha Taifa cha
Ulinzi cha Kenya (National Defence College) kilichoko Karen, Nairobi, ambako
atapokelewa na Waziri wa Nchi wa Ulinzi, Mheshimiwa Yusuf Haji na Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi.
Baadaye,
Rais Kikwete atakwenda kutembelea Kituo cha Magonjwa ya Moyo na Kansa kwenye
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ambako atapokelewa na Waziri wa Huduma za
Matibabu, Mheshimiwa Anyang Nyong’o.
Baadaye
jioni, Rais Kikwete, ambaye anaongozana na kundi kubwa la Wafanyabiashara wa
Tanzania, atashiriki chakula cha jioni ambacho ameandaliwa na Jumuiya ya Wafanya
Biashara ya Kenya.
No comments:
Post a Comment