Dawati la Mhariri

Na Joyce Mwakalinga




Juni 21 mwaka huu katika hospitali ya Mwananyamala ya jijini Dar eS Salaam kumetokea tukio la kusitikisha na la kushtua kufuatia kuibiwa kwa mwili wa kichanga muda mfupi baaya ya kuzaliwa na mwanamke mmoja mkazi wa Mburahati jijini humo.

Tukio hilo lilithibitishwa na wazazi wa kichanga hicho, ndugu pamoja na Hospitali husika ambayo naweza kusema imeingia katika kashfa nyingine kufuatia tukio hilo.

Kwa mujibu wa wanafamilia wa mzazi wa mtoto huyo wanasema ndugu yao huyo Bi.Sara Ibrahim alifika hospitalini hapo alfajiri ya Juni 21 na bila kukawia alijifungua mtoto akiwa tayari amefariki.


Baada ya tukio hilo baadhi ya ndugu wakishirikiana na baba wa mtoto walichukua maiti ya mtoto wao na kuiviringisha kwenye kanga kwa ajili ya kuitambua kwa urais pale itakapochanganywa na maiti nyingine, jitihada ambazo hazikuzaa matunda na mwili huo kutoonekana.

Hata hivyo mwanamke huyo alibaki akiwa amelazwa katika wodi namba 1B kuwaruhusu ndugu zake kwenda kutoa taarifa polisi ili kufanyika uchunguzi wa kina utakaosaidia upatikanaji wa mwili huo.

Familia hiyo tayari imefungua kesi katika kituo cha polisi Oysterbay na kupewa RB namba 0B/RB/11351/2012.

Pamoja na hatua zilizochukuliwa lakini swali la kujiuliza maiti hiyo imechukuliwa na nani? Kwa madhumuni gani? Wizi huu unatia shaka sana.

Ni vema uongozi katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Mwanayamala kuwa makini na vitu vya muhimu kama hivyo, pengine hakukuwa na wazo kama kunaweza tokea wizi kama huo lakini sasa ni nafasi ya kujifunza kwa wakati mwingine lisitokee tena jambo kama hilo.

Pamoja na kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na mkasa huo, mamlaka husika likiwemo jeshi la polisi zinapaswa kashughulikia suala hili hadi itakapofahamika na kumchukulia hatua za kisheria aliyehusika kwa namna moja ama nyingine na kuwa fundisho kwa wengine.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment