Sunday, July 29, 2012

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA JOEL BENDERA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Joel Nkaya Bendera kuomboleza kifo cha Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kilosa, Alhaj Shaweji Abdallah, ambaye pia alipata kuwa mjumbe wa miaka mingi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi.

Katika salamu zake kufuatia hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Jumapili, Julai 29, 2012, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Bendera: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Alhaji Shweji Abdallah ambaye alikuwa mtumishi wa miaka mingi wa umma na ambaye nimejulishwa kuwa alifariki dunia usiku wa kuamkia leo.”

“Alhaj Shaweji Abdallah alikuwa mtumishi mfano wa kuigwa wa utumishi wa umma. Katika kazi zake zote alizopata kuzifanya kama vile uongozi wake katika sekta ya kilimo cha katani, ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya chama changu, Mheshimiwa Shaweji Abdalla alionyesha uzalendo na uadilifu wa kiwango cha hali ya juu.”

Amesisitiza Mheshimiwa Rais: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo cha Mzee wetu ambaye ameaga dunia tukiwa bado tunahitaji busara zake. Kupitia kwako pia nawatumia wana-familia pole nyingi kwa kuondokewa na mhimili wa familia yao. Waambie moyo wangu uko nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke pema peponi roho ya Alhaj Shaweji Abdallah. Amen.”

No comments:

Post a Comment