Registrar Prof. Dr. John Eudes Ruhangisa |
Na Mboneko
Munyaga, EANA
Arusha, 1 Juni,
2012 (EANA) – Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) yatapanuliwa katika
siku za usoni kushughulikia pia kesi za makosa ya jinai zikiwemo za mauaji ya
kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.
Msajili wa Mahakama
hiyo Profesa John Ruhangisa aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika
Mashariki (EANA) katika mahojiano maalum kwamba mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa
maelekezo ya kikao cha hivi karibuni cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC).
“ Ni kweli kwamba
upanuzi wa mamlaka ya Mahakama hii yatahusisha pia mashitaka ya uhalifu dhidi ya
binadamu na hii ni kwa mujibu wa maelekezo ya Kikao cha Wakuu wa Nchi
wananchama. Inamaanisha kwamba Mahakama hii itakuwa na uwezo wa kushughulikia
mashitaka kama vile ya mauaji ya kimbari na mengine kama vile ya watuhumiwa wa
Kenya ambayo kesi yake sasa ipo mbele ya ICC( Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai),” Profesa Ruhangisa alifafanua.
Vyote viwili,
Mahakama na Afrika Mashariki vina majaji wenye uwezo wa kushughulikia kesi za
aina hii, alisema katika mahojiano ambayo yatachapishwa hivi karibuni. Mahojiano
hayo yaliyofanyika katika lugha ya Kiingereza, pia yatapatikana katika lugha za
Kiswahili na Kifaransa kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya
kanda.
Lakini alikiri pia
kwamba kuna vikwazo. Alisema upatikanaji wa rasilimali watu na fedha za
kugharimia upanuzi huo ni miongoni mwa changamnoto iliyopo. Mambo haya
yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi kwanza, aliongeza.
Alifafanua kwamba
ili mahakama iweze kushughulikia kesi za jinai kunahitajika kuanzishwa kwa idara
mbalimbali ikiwa ni pamoja na za mwendesha mashitaka, upelelezi, ulinzi wa
mashahidi na magereza.
“ Inawezekana
kiufundi na kiutekelezaji lakini masuala mengi yanahitajika kufanyiwa kazi na
kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuelekea rasmi upande huo,” alishauri.
Iwapo EACJ itafanikiwa kufikia hatua hiyo ya
upanuzi wa mamlaka yake kushughulikia kesi za jinai, itakuwa imelamba ‘bingo’ ya
hatma yake ya kuweza kushughulikia matatizo yake yenyewe katika kanda ya EAC. Na
pia kamwe kutoshuhudia tena mauaji yaliyotokea Rwanda na Kenya.
Hivi sasa EACJ
inashughulikia mashauri yanayohusu zaidi madai.
No comments:
Post a Comment