Thursday, July 12, 2012

ZAIDI YA WATU 10 WAFARIKI KWA GONGO


JESHI la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni limesema linafanya uchunguzi wa vifo vya zaidi ya watu kumi wanaodaiwa kufa baada ya kunywa pombe haramu aina ya gongo inayosadikiwa kuchanganywa na spiriti pamoja jiki.


Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni  Charles Kenyela
Uandaaji wa gongo (Picha: simbadeo.wordpress)

Vifo hivyo vya mashaka vinadaiwa kutokea kati ya Julai 9 hadi 12, mwaka huu katika maeneo ya Kigogo Mbuyuni huku wagonjwa wengine nane wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi kufuatia madhara yanayotokana na pombe hiyo.

Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela amesema kuwa bado jitihada za ziada zinahitajika za kudhibiti uuzwaji wa pombe haramu kutokana na uwepo wa mianya kwenye sheria za nchi.
Naye Mkuu wa Kitengo Cha Dharura katika Hospitali ya Amana Christopher Mzava amesema kuwa idadi ya wagonjwa hao imeongezeka kutoka 9 hadi 12.

Hata hivyo wakazi wa eneo hilo wanabainisha kuwa kupanda kwa gharama za maisha kunachochea ongezeko la unjwaji wa pombe hiyo haramu kutokana na watu kushindwa kumudu gharama za pombe zilizothibitishwa.

Miongoni mwa watu hao waliofariki dunia kufuatia madhara ya pombe hiyo ni pamoja na Mama anayedaiwa kuuza pombe hiyo Hekima Bakari ambaye alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Amana chini ya ulinzi mkali wa polisi.

No comments:

Post a Comment