Wednesday, July 25, 2012

WAPIGAPICHA WATAKIWA KUPIGA PICHA ZENYE KULETA TIJA KWA MTANGAMANO WA EAC



Na Nicodemus Ikonko, EANA

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk. Julius Rotich ametoa wito kwa wapiga picha wa kanda hiyo kutumia ujuzi na taaluma yao kuhamasisha umma juu ya masuala ya mtangamano na ya Afrika kwa ujumla wake.

Akifungua warsha ya siku tatu ya wapiga picha kutoka nchi tano wananchama wa jumuiya hiyo jana, Dk. Rotich hakumung’unya maneno yake kwa kuonyesha wazi kwamba mara nyingi watu wa nje ya bara la Afrika hulionyesha bara hilo kupitia picha kuwa limejaa magonjwa, njaa na migogoro tupu.

‘’Wakati umefika sasa kwa sisi wenyewe kuchukua changamoto hiyo kwa kuionyesha kanda yetu kuwa imejaa matumaini, fursa za kuwekeza, ni kitivo kimoja kikubwa cha utalii na uwekezaji kwenye nyanja hiyo na kwamba ni watu wamoja wenye mstakabali mmoja,’’ alisisitiza.

Dk. Rotich aliendelea kueleza kuwa ‘’tunahitaji kuweka kumbukumbu na kulinda mchakato mzima wa mtangamano, kuelezea watu wetu wa aina mbalimbali, maisha yao na utamaduni wa Afrika Mashariki.’’

Aliwakumbusha washiriki wa warsha hiyo msemo maarufu usemao, ‘’picha hueleza maneno elfu,’’ na kuwataka wataalamu hao kutumia usemi huo kuwaelimisha na kuwahabarisha raia wa kanda hiyo juu ya hatua za mafanikio yaliyofikiwa katika mtangamano wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Dk. Rotich wapiga picha na vyombo vya habari kwa ujumla wake vinaweza kuleta msukumo wa aina yake katika masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kanda hiyo yenye jumla ya nchi tano ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
‘’Kuhamasisha na kutoa tafsiri ya masuala mbalimbali ya EAC, maoni, kupanga ajenda na ujenzi wa hoja vinaweza kufanyika kwa urahisi zaidi kwa kutumia ‘’nguvu ya lensi ya kamera,’’ alisisitiza.

Aliwaonya washiriki wa warsha hiyo kuachana na masuala ya upotoshaji wa uhalisia wa picha wanazopiga na maelezo yanayoambatana nayo, huku akielezea matumaini yake kuwa warsha hiyo itasaidia kuboresha utendaji wao katika sekta hiyo.

Warsha hiyo umeandaliwa na EAC kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendelea la Ujerumani (GIZ) ambalo Dk. Rotich amelishukuru kwa kuunga mkono uwezeshwaji wa wake.

No comments:

Post a Comment