Na Juma Mohammed,
MAELEZO Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia
Julai 19 hadi Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit
iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein
akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na
kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za
maombolezo.
Dk. Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. Katika
taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein
amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba
gharama zote za mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.
“Nimesikitishwa sana na msiba huu, Katika wakati huu si vema tukaanza
kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu” Alisema
Rais Dk. Shein.
Mbali ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti
zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.
Mbali ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya
Zanzibar kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania jana lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo wakati wa
jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya
majumuisho ya bajeti yake.
Baadhi ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa,Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi katika
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti
hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.
Mbali ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda
shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika
shughuli za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi
mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.
Taarifa kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti
30 zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa zao
huku wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa katika
eneo la Maisara.
Aidha, katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo
katika hali nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa
matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea
Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima,
watoto 31 na mabaharia 6.
Kazi ya utafutaji na uokoaji zinaendelea
asubuhi hii katika eneo la tukio ilikozama meli hiyo umbali wa maili sita
Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
No comments:
Post a Comment