Sunday, July 15, 2012

MKURUGENZI MKUU MTENDAJI TANESCO ASIMAMISHWA

Mhandisi William Mhando
Mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika la ugavi wa umeme nchini TANESCO Mhandisi William Mhando amesimamishwa na bodi ya shirika hilo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka dhidi yake kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa na bodi hiyo na kusainiwa na mwenyekiti wake Jenerali mstaafu Robert Mboma. Uamuzi huo ulitokea jana jioni baada ya bodi hiyo kukaa kikao cha dharura.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa tuhuma hizo dhidi ya mhandisi Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa kina kama inavyoeleza, "Hivyo, bodi iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini".

Pamoja na mhandisi huyo, viongozi wengine wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi huo wakiwemo Robert Shemhilu ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Ofisa Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Manunuzi Harun Mattambo.


No comments:

Post a Comment