Wednesday, July 4, 2012

HALI YA MASHARIKI MWA DRC YAMPA WASIWASI RAIS KIKWETE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatia wasiwasi na hivyo Tanzania inafuatilia kwa makini hali inavyoendelea katika eneo hilo la nchi hiyo jirani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ingependa kuona hali ya amani inarejea katika DRC kwa sababu nchi hiyo inahitaji kupata muda wa amani ili waelekeze nguvu zake kwenye maendeleo badala ya kupigana.
 Rais Kikwete amesema hayo jana, Jumanne, Juni 3, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Profesa Ntumra Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa International Conference on Great Lakes Region (ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca Golf mjini Bujumbura, Burundi.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete alikuwa mjini Bujumbura kushiriki katika Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi na kurejea nyumbani jana, 3 Juni, 2012. Kabla ya kuja hapa, Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali, Rwanda, kushiriki katika sherehe za namna hiyo zilizofanyika Julai Mosi, mwaka huu. Rwanda na Burundi zilipata uhuru kutoka kwa Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2, mwaka 1962.

No comments:

Post a Comment