Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania TPA imewasilisha mapendekezo yake kwa Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA ya kutaka ongezeko la tozo za kuhudumia
meli bandarini kutoka asilimia 4 hadi asilimia 40 ili kukidhi mahitaji ya
ushindani wa kiuchumi.
Ongezeko la tozo hilo limelenga kwenye huduma za Kuegesha meli bandarini, tozo za bandari, tozo za kuongoza meli kuingia bandarini, tozo za kuegesha meli, huduma za kufunga meli getini, tozo za nahodha kuingiza meli bandarini, tozo kwa meli zinazosubiri kazi au maelekezo bandarini, gharama za leseni na ada na tozo za kuhudumia mafuta.
Ni Kaimu Meneja masoko
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA Francisca Muindi akibainisha
sababu za ongezeko hilo na kwamba lina lengo la kuboresha huduma za bandari
bila kuwaumiza watumiaji wake.
Hata hivyo ombi hilo
linapingwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za usafiri wa
Nchi Kavu na Majini Oscar Kikoyo kwa madai kuwa limekiuka kanuni ya Sumatra na
wadau wake ya mwaka 2010 kutokana na
kuleta maombi yasiokuwa na mchanganuo wa sababu za ongezeko la tozo hilo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa
Sumatra Ahmad Kalima ameitaka TPA kuboresha huduma kulingana na kiwango cha
tozo hizo ambacho mtumiaji atakimudu hali itakayosaidia upatikanaji wa huduma
bora zenye kwenda sambamba na ushindani kwenye bandari za nchi za jirani.
Kufuatia suala hilo
Sumatra kwa kushirikiana na wadau wake wa usafiri imefanya mkutano wa kujadili
mapendekezo ya TPA ili kupata muafaka wa suala hilo wenye lengo la kuboresha
upatikanani wa huduma bora zisizomuathiri mtumiaji wa bandari ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment