Wednesday, July 25, 2012

TPA YATAKA ONGEZEKO LA TOZO ZA KUHUDUMIA MELI BANDARINI KUONGEZEKA TOKA 4% -400%

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA imewasilisha mapendekezo yake kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA ya kutaka ongezeko la tozo za kuhudumia meli bandarini kutoka asilimia 4 hadi asilimia 40 ili kukidhi mahitaji ya ushindani wa kiuchumi.

Ongezeko la tozo hilo limelenga kwenye huduma za Kuegesha meli bandarini, tozo za bandari, tozo za kuongoza meli kuingia bandarini, tozo za kuegesha meli, huduma za kufunga meli getini, tozo za nahodha kuingiza meli bandarini, tozo kwa meli zinazosubiri kazi au maelekezo bandarini, gharama za leseni na ada na tozo za kuhudumia mafuta.
Ni Kaimu Meneja masoko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA Francisca Muindi akibainisha sababu za ongezeko hilo na kwamba lina lengo la kuboresha huduma za bandari bila kuwaumiza watumiaji wake.
Hata hivyo ombi hilo linapingwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za usafiri wa Nchi Kavu na Majini Oscar Kikoyo kwa madai kuwa limekiuka kanuni ya Sumatra na wadau wake ya  mwaka 2010 kutokana na kuleta maombi yasiokuwa na mchanganuo wa sababu za ongezeko la tozo hilo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra Ahmad Kalima ameitaka TPA kuboresha huduma kulingana na kiwango cha tozo hizo ambacho mtumiaji atakimudu hali itakayosaidia upatikanaji wa huduma bora zenye kwenda sambamba na ushindani kwenye bandari za nchi za jirani.
Kufuatia suala hilo Sumatra kwa kushirikiana na wadau wake wa usafiri imefanya mkutano wa kujadili mapendekezo ya TPA ili kupata muafaka wa suala hilo wenye lengo la kuboresha upatikanani wa huduma bora zisizomuathiri mtumiaji wa bandari ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment