Friday, June 22, 2012

Serikali yaanza jitihada kuwalinda wakulima wa pamba

 

SERIKALI imeanza jitihada kubwa za kuwalinda wakulima wa zao la pamba nchini kufutilia kuporoka kwa bei ya zao hilo kwenye masoko ya kimataifa.
Ili kuhakikisha kuwa wakulima hao hawaumii kupita kiasi katika hali ya sasa ya mporomoko wa bei ambao ni dhahiri utaathiri bei za zao hilo kwa wakulima nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mfululizo wa mikutano kujadili suala hilo.
Akiwa mjini Dodoma kikazi, Rais Kikwete usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Juni 22, 2012, alifanya mikutano miwili ambako kwanza alikutana na kuzungumza na wanunuzi wa zao la pamba na katika mkutano wa pili akakutana na kuzungumza na wabunge wa maeneo yanayolima pamba nchini wakiongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Ndugu John Cheyo.
Mikutano hiyo miwili imefuatiwa na mkutano wa viongozi wa wakuu wa Serikali uliofanyika asubuhi la leo kwa nia ya kuona ni hatua zipi zinaweza kuchukuliwa angalau kuinua bei la zao hilo kwa wakulima.
Katika msimu uliotarajiwa kuanza mwanzoni mwa wiki hii, wanunuzi wa pamba walikuwa wamesema kuwa watanunua kilo moja ya pamba kwa kiasi cha sh. 525 kulinganisha na bei ya mwaka jana ya sh. 1,200 kwa kilo moja.
Bie hiyo imepingwa kwa kiasi fulani na wabunge kutoka maeneo yanayolima pamba ambao wamekuwa wanawataka wakulima wa zao hilo wasikubali kuuza pamba yao chini ya sh. 1,000 kwa kilo moja.
Jitihada za Serikali zinalenga kuona jinsi gani kiasi hicho cha sh. 525 kinaweza kupanda angalau kufikia sh. 725 na hivyo kukaribia kabisa bei ya sh. 800, ambayo wakulima walilipwa mwanzoni mwa msimu wa mwaka jana, kabla ya kiwango hicho kupanda na kufikia 1,200 kwa kadri bei ya pamba duniani ilivyozidi kupanda.
Serikali inaona kuwa siyo vyema wala siyo haki kwa mkulima wa pamba kubebeshwa mzigo wote wa kuporomoka kwa bei ya zao hilo duniani badala ya mzigo huo kugawanywa mionogni mwa wadau wengine wa zao hilo.

No comments:

Post a Comment